ALIYEKUWA mwanafunzi mzee kuliko wote duniani, Kimani Maruge amefariki Ijumaa wiki hii, katika hospitali ya Nairobi alipokuwa akipata matibabu ya kansa. Maruge( 84), alifanya tukio la kihistoria pale alipoamua kujiunga na shule ya msingi Kapkenduiywo iliyopo Mashariki mwa Kenya, mwaka 2004 kufuatia kuanzishwa kwa utaratibu wa elimu bila malipo , ulianza rasmi mwaka 2003 chini ya chama cha Narc.
Katika enzi za uhai wake, Maruge alikuwa na malengo ya kuwa Daktari mwenye umri mkubwa. Mwaka 2008, alikuwa mmoja kati ya maelfu ya watu walioshindwa kurejea masomoni kutokana na vurugu za uchaguzi zilizotokea nchini humo,nyumba pamoja na mali zake ziliharibiwa vibaya na wapinzani.
Eneo la Langas Estate, ambapo ndipo alikuwa akiishi kuliathiriwa vibaya na vurugu hizo, iliripotiwa kuwa jumla ya watu 11 waliuawa nyumba ya pili kutoka kwake Disemba 30,2008. Maruge alifanikiwa kutoroka kutoka Eldoret hadi Nairobi kutokana na kutokuwepo na hali ya usalama huko nyumbani kwake.
Shirika la msalaba mwekundu nchini humo walimtafutia makazi katika nyumba ya wazee inayofahamika kama Chesire iliyopo jijini Nairobi. Muda mchache baada ya kuishi Nairobi aligunduliwa kuwa na kansa ya utumbo.
Maruge, ambaye ameweka rekodi katika kitabu cha Guinness ya kuwa mwanafunzi mwenye umri mkubwa zaidi kujiunga na elimu ya msingi.
Rekodi hiyo alichaguliwa kushika nafasi hiyo akiwa darasa la tano mwaka 2007, ambapo katika mtihani wake wa mwisho wa mwaka alishika nafasi ya 14 kati ya wanafunzi 58 waliofanya mtihani huo.
Akiwa shuleni hapo alisema taaluma aliyoipata imemsaidia sana kuongeza uelewa kwani hadi wakati huo aliweza kusoma vizuri biblia.Somo la Kiswahili ndio lilikuwa chaguo lake.
Jane Obinchu ambaye alikuwa ni mwalimu wake ni miongoni mwa watu waliotoa salamu za rambirambi kwa familia ya marehemu Maruge.